Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yaanzisha kampeni ya chanjo kwa mifugo huko Mosul

FAO yaanzisha kampeni ya chanjo kwa mifugo huko Mosul

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa , FAO limezindua kampeni ya dharura ya chanjo kwa  wanyama katika eneo la Mosul  jimbo la Ninewa nchini Iraqi, ambalo hivi karibuni limekombolewa  kutoka  kwenye kundi la wanamgambo la Kiislamu  (ISIL).

Kampeni hiyo inaotekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo ya Iraq, inalenga kondoo milioni 1, mbuzi, ng'ombe na nyati halikadhalika kusambaza chakula cha mifugo chenye virutubisho.

Kampeni hiyo itaokoa wanavijiji wapatao 210,000 ambao wanategemea mifugo kama chanzo cah mapato jimbo hilo la Ninewa.

Paul Schlunke ni mratibu wa dharura wa FAO nchini Iraq.

(Sauti ya Paul)

 “Tutajikita sana maeneo ambayo yalikuwa ngome ya ISIL, mifugo mingi  katika vijiji vya maeneo hayo imehamishwa na kupelekwa vijiji vingine kutokana na hali ya kiusalama. Mifugo mingi imeathirika sana kwasababu haijapewa chanjo kwa muda mrefu kutokana na migogoro iliyoikumba eneo hilo, hivyo kusababisha wafugaji wengi watelekeze au wauze mifugo yao ili kujipatia kipato. Tunachokifanya sasa ni kutoa chanjo kwa mifugo iliosalia ili wafugaji wapate  mifugo iliyo na afya njema iwasaidie katika mahitaji yao ya kila siku”

FAO inasema chanjo hiyo pia itaepusha kuenea kwa magonjwa ya mifugo ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi na afya kwa umma.

Jimbo la Ninewa limeathiriwa sana na migogoro tangu ulipokuwa chini ya utawala wa ISIL mwaka 2014 ambapo zaidi ya watu milioni moja ni wakimbizi wa ndani na mifugo yao haijatibiwa tangu ISIL watwae eneo hilo.