Baraza la usalama la UM limelaani mashambulizi ya kigaidi El Wahat Misri

22 Oktoba 2017

Wajumbe wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea tarehe 20 Oktoba katika jangwa la El Wahat Misri, na kukatili maisha ya watu kadhaa wa vikosi vya usalama na wengi wao kujeruhiwa.

Baraza hilo limetuma salamu za rambirambi kwa serkali ya Misri na kwa familia za waathirika huku ikiwatakia ahueni majeruhi katika kipindi hiki kigumu.

Pia baraza limeiasa serikali ya Misri na mamlaka zingine husika, kuwachunguza wahalifu, waandaaji, wafadhili na wadhamini wa vitendo hivyo vibaya na kuwachukulia hatua za kishereia kwa mujibu sheria za kimataifa na maamuzi ya Baraza la Usalama .

Aidha wajumbe wa baraza la usalama wametoa wito kwa Mataifa yote kushirikiana kwa njia zote katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa , chini ya sheria ya kimataifa za haki za binadamu, sheria ya kimataifa ya wakimbizi na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kuhusu vitisho vya amani na usalama wa kimataifa unaosababishwa na vitendo vya kigaidi.