UNICEF yaonya juu ya madhila ya wototo kambini, Bangaladesh

20 Oktoba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, linasikitishwa na madhila yanaowakumba maelfu ya watoto kambini Kusini mwa Bangladeshi, kufuatia operesheni za kijeshi zilizoshuhudiwa majuma kadhaa yaliopita.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNICEF, kufuatia operesheni ya usalama katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar zaidi ya nusu ya watu laki sita waliowasili Bangladesh katika wiki chache zilizopita ni watoto.

Hali ya watoto ikiezwa kutotia matumaini, UNICEF imesema waliohatarini zaidi ni wale zaidi ya 10,000 waliowasili Bangaladeshi hivi karibuni kutoka Myanmar, huku changamoto kubwa zaidi ikiwa ni uhaba wa maji safi.

Baada ya kutembelea maeneo ya Cox’s Bazar Bangladesh, ambako maelfu ya Waisilamu wa jamii ya wa Rohingya kutoka Myanmar wamekuwa wakikimbilia, Simon Ingram msemaji wa UNICEF anasema

(INGRAM CUT)

Kisa kimoja ambacho ninakumbuka ni kisa nilichosimuliwa na mvulana mmoja ambaye alichora picha aliyowasilisha kwetu, ilikuwa inaonyesha mtu aliyevalia sare akikata koo ya mtoto aliyekuwa amelala sakafuni. Hiki ni kitu alichoshuhudia kwa macho yake mwenyewe.”

Ameonya kwamba hali ya watoto itazoroka zaidi endapo Umoja wa Mataifa hautafanikiwa katika ombi lake la mchango wa dola milioni 430 kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, Myanmar.

(INGRAM CUT 2)

“Kufikia Agosti 25 kulikuwa na programu zinazoendelea ambazo zilikuwa zinawafikia watoto waliokuwa hatarini zaidi katika jimbo la Rakhine Kaskazini na sisi tunatoa wito kwa mamlaka nchini Myanmar kuturuhusu kurejea. Zaidi ya hapo sina uhakika kuhusu kile ambacho tunaweza kufanya, ni lazima tuendelee kupaza sauti, hatuwezi kukaa kimya.”

Hali kwa Warohingya vijijini bado ni tete wakiendelea kuvuka mpaka kuelekea Bangladesh na kusimulia visa vya ghala la chakula kuharibiwa kwa maksudi.