Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ya kudumu Afrika itapatikana kwa kujumuisha wa mashinani- Balozi Mulamula

Amani ya kudumu Afrika itapatikana kwa kujumuisha wa mashinani- Balozi Mulamula

Wiki ya Afrika kwenye Umoja wa Mataifa ikikaribia ukingoni jijini New York, Marekani, imeelezwa kuwa jitihada za pamoja zisizoengua watu wa mashinani ndio muarobaini wa amani, utulivu na maendeleo barani humo.

Balozi Liberata Mulamula, ambaye ni Mkuu wa Idara ya masomo ya Afrika kwenye Chuo Kikuu cha George Washington, nchini Marekani amesema hayo wakati wa kikao cha ngazi ya juu kuhusu mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji na uhusiano wake na masuala ya amani na utulivu barani Afrika.

Akiwa ni mmoja wa wazugumzaji wakuu kwenye kikao hicho, Balozi Mulamula amesema..

(Sauti ya Balozi Mulamula)

“Ushahidi unaonyesha kuwa wanawake na vijana ndio wahanga wa kwanza mwa athari za mabadiliko ya tabianchi wakati wa mizozo, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na hali ngumu ya kiuchumi. Wanawake pia ni mawakala wazuri wa kuleta mabadiliko chanya kwa mtazamo wa kutumia ujuzi wa kiasili ambao unaweza kutumika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Balozi Mulamula ambaye pia ni mjumbe wa mtandao wanawake viongozi barani Afrika ulioanzishwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ametolea mfano bonde la ziwa Chad ambako kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi tayari wanawake wamechukua hatua kuweza kumudu kuishi na kulea familia zao, hivyo amesema..

(Sauti ya Balozi Mulamula)

“Sote tunafahamu sababu, hoja ni nini, na jinsi ya kutatua kupitia juhudi na makubaliano mengi ya kimataifa. Tunahitaji kujenga uhusiano bora kati ya binadamu na sayari dunia kwa ajili ya maendeleo endelevu na amani na utulivu wa kudumu.”