Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wachanga 7,000 walifariki dunia kila siku mwaka 2016- Ripoti

Watoto wachanga 7,000 walifariki dunia kila siku mwaka 2016- Ripoti

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF inaonyesha kuwa mwaka jana watoto 15,000 walifariki dunia kila siku maeneo mbalimbali ulimwenguni kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Ikipatiwa jina viwango na mwenendo wa vifo vya watoto ya mwaka 2017, ripoti inasema asilimia 46 kati yao hao ni watoto wachanga ambao walifariki dunia kabla hata ya kufikisha mwezi mmoja.

Ripoti inataja magonjwa yaliyoongoza kwa kusababisha vifo hivyo vya watoto kuwa ni vichomi na kuhara.

Ingawa idadi ya vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano inaonekana kupungua mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2000 bado kiwango cha vifo miongoni mwa watoto wachanga ni kikubwa.

image
Mama akiwa na mwanae mchanga katika taasisi ya afya huko Dhaka, Bangladesh. Katika kituo hiki, wazazi ambao wana mahitaji maalum wanasaidiwa ili kuhakikisha afya yao na watoto wao. (Picha:UN/Kibae Park)
Eneo la Kusini mashariki mwa Asia linaongoza kwa kuwa na asilimia 39 ya vifo vyote vya watoto wachanga, likifuatiwa na nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara.

Dkt. Flavia Bustreo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Msaidizi masuala ya familia amesema ili kufanikisha mipango ya afya kwa wote na kuhakikisha kuwa watoto wachanga wanakua na kustawi ni lazima kusaidia familia zisizo na uwezo.

Sambamba na hilo ni kuinua uwezo wa kipato cha familia ili ziweze kuepukana na magonjwa na kupata huduma sahihi kabla, wakati na hata baada ya mama kujifungua.