Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano Palestina ni muhimu kwa ajili ya amani endelevu- Jenča

Makubaliano Palestina ni muhimu kwa ajili ya amani endelevu- Jenča

“Rais na wanachama wa Baraza la Usalama, kikao cha leo ni muhimu kwani kinalenga kumaliza mzozo wa takriban muongo mmoja wa mgawanyiko nchini Palestina na kurejesha Gaza kwa uongozi halali wa mamlaka Palestina.”

Hivyo ndivyo ilivyoanza hotuba yakeMsaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu maswala ya kisiasa Miroslav Jenča akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limekutana leo kujadili hali Mashariki ya kati.

Bwana Jenča ameliambia Baraza la Usalama kwamba makubaliano kati ya mamlaka ya Palestina ikiongozwa na Fatah katika ukingo wa Magharibi na kundi la Hamas linalosimamia ukanda wa Gaza ni muhimu kwa ajili ya kufikia makubaliano ya amani ya kudumu kati ya Palestina na Israel.

Ameongeza kuwa hali ya wakaazi milioni mbili wa Gaza inaendelea kuzorota huku wakikosa huduma muhimu na wakipata umeme kwa saa chache tu. Aidha mitaro ya maji taka inaelekea Mediterranea na kuweka hatari ya kimazingira isiyo na mipaka.

Akizungumzia umuhimu wa makubaliano hayo  amesema…

(Sauti ya Jenča)

“Makubaliano ni hatua muhimu kuelekea lengo la umoja wa Palestina, chini ya mamlaka moja ya kidemokrasia ya Palestina, Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na viongozi wa Palestina na katika ukanda huo, ili kuunga mkono mchakato huu, ambao ni muhimu katika kupata suluhi ya mataifa mawili na amani endelevu.”

Viongozi waliojihami wa kundi la Hamas waliishurutisha Fatah kuondoka Gaza mwaka 2007, na makubaliano yaliofikiwa Cairo wiki jana yatawezesha mamlaka ya Palestina kurejelea usimamizi wa mipakani.