Idadi ya watoto waliounganishwa na familia zao Sudan Kusini yafikia 5000

18 Oktoba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema zaidi ya watoto 5000 wameunganishwa na familia zao tangu mzozo uibuke nchini Sudan Kusini mwezi disemba mwaka 2013,.

UNICEF imesema katika taarifa yake kuwa idadi hiyo imefikia hivi karibuni baada ya mtoto wa 5,000 mwenye umri wa miaka 17 ambaye alitoroka mji wa Tombura ulioko jimbo la Equatoria Magharibi na kusaka hifadhi huko Wau.

Mtoto huyo ameunganishwa na mama yake mzazi baada ya kutengana naye kwa miaka ipatayo minne.

Mwakilishi wa UNICEF huko Sudan Kusini Mahimbo Mdoe amesema kuweka familia pamoja ndio njia pekee ya kuhakikisha watoto wanalindwa na ndio maana mchakato wa kufuatilia watoto na kuunganisha na familia zao ni jambo muhimu.

Bwana Mdoe amesema watoto wanategemea familia kwa ajili ya utulivu, ulinzi na usaidizi na mambo hayo ni muhimu zaidi wakati wa mizozo.

Amesema kadri mtoto anapokuwa mbali na familia, ndio anakuwa hatarini zaidi kukumbwa na madhila kama vile ukatili wa kingono, unyanyasaji na usafirishaji haramu.

Mtoto huyo ambaye jina lake halikutajwa ameshukuru UNICEF kwa kuweza kumuunganisha na familia yake.