Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za IMF za ukopeshaji zinadumaza maendeleo- de Zayas

Sera za IMF za ukopeshaji zinadumaza maendeleo- de Zayas

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji wa demokrasia na utulivu wa kimataifa Alfred de Zayas ameonya kuwa sera za ukopeshaji za shirika la fedha duniani, IMF zinasigina baadhi ya vipaumbele vya haki za binadamu na maendeleo.

Bwana de Zayas amesema hayo akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akisema kuwa sera hizo zimechochea kushindwa kwa mipango ya ubinafsishaji na kupunguza matumizi.

Ametoa mfano kuwa IMF inaweka masharti kwa nchi kutopatia kipaumbele matumizi ya fedha kwa huduma za kijamii na hivyo kufanya serikali zisishindwe kutimiza wajibu wake wa kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

Sambamba na hilo sera hizo zinaongeza ukosefu wa ajira, zinashusha viwango vya sheria zinazosimamia ajira, mazingira na kupunguza uwezo wa wananchi kupata elimu bora.

Kwa mantiki hiyo Bwana de Zayas amependekeza sera bora za ukopeshaji ambazo zinachagiza nchi kusimamia ahadi zao za haki za binadamu na maendeleo badala ya mipango inayokwamisha ahadi hizo.

Ametaka IMF na Benki ya Dunia wafanye kazi kwa karibu zaidi na mfumo wa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha maendeleo endelevu badala ya sera zao kuwa kikwazo.