Mwelekeo wa kikosi cha kikanda Sudan Kusini unatia matumaini- Lacroix

17 Oktoba 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuwa harakati za kupeleka kikosi cha  ulinzi cha kikanda, RPF huko nchini Sudan Kusini, zinaendelea na zinatia matumaini.

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amesema hayo leo alipohutubia Baraza hilo ikiwa ni ripoti ya Katibu Mkuu anayotakiwa awasilishe kila baada ya siku 30.

Amesema kikosi kamili cha askari wa miguu kutoka Rwanda kitakamilika mwezi  ujao huku kikosi cha Ethiopia tayari kimeanza kuwasili mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, na hivyo kuongeza doria katika maeneo ambayo awali ilikuwa ni vigumu kufika.

Kuhusu hali ya usalama amesema bado inatia hofu katika maeneo ya Jonglei Kaskazini, Equatoria kati ya askari wa jeshi la serikali la SPLA na wapiganaji wa waliojitenga wa SPLA upande wa upinzani wanaomuunga mkono Riek Machar.

(Sauti ya Lacroix)

“Hali ya kibinadamu nchini humo inatia wasiwasi sana. Mauaji ya raia yanafanyika kinyume cha sheria, watu wanakamatwa hovyo na kushikiliwa korokoroni, uhuru wa kujieleza umebinywa na manyanyaso dhidi ya wapinzani wa kisiasa yameripotiwa wakati huu.”

Akizungumzia uwezo wa watendaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo Bwana Lacroix amesema..

(Sauti ya Lacroix)

“Vyombo vya dola vimeendelea kudhibiti uhuru wa UNMISS kutekeleza shughuli zake. Vivyo hivyo, vikosi vya wapiganaji waliojihami wanadhibiti uingiaji wa maeneo ambayo wanadhibiti. Hivy basi nasihi Baraza la Usalama litoe kauli yake ya kuhusu ukiukwaji wa makubaliano ya SOFA kwani vikwazo hivyo vya serikali na waliojihami vinatia wasiwasi mkubwa.”

Bwana Lacroix amesihi pia Baraza hilo litumie uwezo wake kushawishi pande kinzani Sudan Kusini kurejea katika mazungumzo na kutekeleza mkataba wa amani akisema ndio suluhu pekee ya mzozo huo.