Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasaidia utoaji wa chanjo dhidi ya homa ya manjano Nigeria

WHO yasaidia utoaji wa chanjo dhidi ya homa ya manjano Nigeria

Kampeni ya siku 10 ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano inaendelea kwenye majimbo ya Kwara na Kogi nchini Nigeria.

Serikali ya Nigeria ilizindua rasmi kampeni hiyo siku ya Ijumaa ikilenga watu zaidi ya Laki Nane na Nusu.

Walengwa ni watoto wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi watu wazima wenye umri wa miaka 45.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesaidia kampeni hiyo ambapo mwakilishi wake nchini Nigeria Dkt. Wondimagegnehu Alemu amesema lengo ni kuhakikisha watu walio kwenye maeneo hatari zaidi wanapatiwa chanjo hiyo.

WHO na wadau wa afya wamekuwa wakisaidia serikali ya Nigeria kudhibiti ugonjwa huo tangu mlipuko uripotiwe kwenye jimbo la Kwara tarehe 12 mwezi uliopita.

Tayari shirika hilo limepeleka wataalamu wa kusaidia ufuatiliaji na uchunguzi kwenye maabara pamoja kuweka kituo cha dharura iwapo kuna lolote litahitaji hatua za dharura.

Mara ya mwisho homa ya manjano iliripotiwa Nigeria mwaka 2002 ambapo kati ya visa 20 watu 11 walifariki dunia.