Afrika inasonga mbele, changamoto ni kulinda mafanikioa- Guterres

16 Oktoba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza katika ufunguzi wa wiki ya Afrika kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akisema bara hilo limepiga hatua kubwa katika siku za hivi karibuni.

Ametolea mfano harakati za kupunguza umaskini, kupungua kwa idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wachana, kupanua wigo wa vyanzo vya kuinua uchumi kupitia sekta za mawasiliano, benki, biashara za rejareja na kuweka fursa za kuongezeka kwa idadi ya watu wa daraja la kati.

Amesema hatua hizo ndio zinapaswa kupigiwa chepuo na kuondoka na taswira hasi ya bara hilo na badala yake kuona Afrika kuwa ni bara la fursa.

(Sauti ya Guterres)

“Changamoto yetu ya pamopja na kuendeleza mafanikio haya na kupata mengine zaidi. Hii ndio nia  ya ubia wa dhati na unaoendelea kukua kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa ambao Rais wa Baraza Kuu amezungumzia. Na hii ndio chanzo cha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu na ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika yenye matarajio makubwa.”

Kuhusu jinsi ya kuimarisha na kuendeleza maendeleo endelevu huku fursa zikipanuliwa ili kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma, Katibu Mkuu amesema…

(Sauti ya Guterres)

“Mosi jikiteni zaidi kwa vijana, tunaweza kutumia idadi yao kubwa na kunufaika kwa kuwekeza kwenye elimu hasa sayansi na teknolojia. Pili wezesheni wanawake na wasichana wa Afrika na tatu lazima tuwe wabunifu katika kutumia vyema rasilimali na kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud