Leo ni siku ya mwanamke wa kijijini:
Leo ni siku ya mwanamke wa kijijini ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 15. Katika ujumbe maalumu kwa ajili ya siku hii mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Phumzile Mlambo Ngcuka amesema wanawake na wasichana ni kiungo muhimu cha maendeleo kijijini kuanzia katika familia zao n hata katika jamii, kuboresha maisha ya kijijini na ustawi kwa ujumla lakini mara nyingi jukumu na umuhimu wao huwa unasahaulika.
Na ukweli ni kwamba wanawake hao ni takribani nusu ya nguvu kazi katika mataifa yanayoendelea ikiwa ni pamoja na kuchukua sehemu kubwa ya ajira zisizo na malipo kama kutoa huduma na kazi za majumbani katika familia.
Amesema wanawake hawa wanalima sanjari na wanaume lakini hawafaidiki na mazao yao katika suala la bei, lakini pia wengi hawana fursa ya kumiliki ardhi, kupata mikopo, kuwa na sauti katika masoko na katika mfumo mzima wa chakula.
Sasa kwa pamoja UN Women, shirika la chakula na kilimo FAO, Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD na shirika la mpango wa chakula duniani WFP wanashirikiana kubadili hali hiyo.
Wanawake wa kijijini ni karibu robo ya watu wote duniani na wengi wa asilimia 43 ya wanawake wote ni wakulima.