Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Myanmar: Kofi Annan awasilisha mapendekezo yake UM

Myanmar: Kofi Annan awasilisha mapendekezo yake UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ilivyo nchini Myanmar wakati huu ambapo idadi ya waislamu wa kabila la Rohingya waliokimbilia Bangladesh kukwepa mateso imefikia 536,000.

Kikao hicho kilichoitishwa na Ufaransa na Uingereza kilikuwa cha faragha na wajumeb walipatiwa ripoti ya kamisheni ya ushauri iliyoundwa kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuboresha hali ya kibinadamu kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Baada ya kikao, mwenyekiti ya kamisheni hiyo Kofi Annan akazungumza na waandishi wa habari..

(Sauti ya Kofi Annan)

“Kila mtu amekubali kile kinachopaswa kufanywa sasa. Kusitisha ghasia, kuwasilisha misaada kwa wahitaji, na kusaidia wale wanaotaka kurudi kwa hiari waweze kufanya hivyo kutoka Bangladesh tena kwa utu. Hii haitakuwa rahisi, watarejea tu iwapo watakuwa na imani ya usalama wao na kwamba  maisha yao yatakuwa bora. Na katika ripoti yetu tunasema wasiwekwe kwenye kambi bali waruhusiwe kurudi kwenye vijiji vyao na wasaidiwe kwenye ujenzi mpya."

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa akaenda mbali zaidi kusema kuwa..

(Sauti ya Kofi Annan)

“Jambo muhimu ni kwamba wamekubali hii ripoti, na ripoti hii kwa ujumla imekubaliwa na nchi wanachama, wadau wa masuala ya kibinadamu na maendeleo na mashirika ya kiraia. Hii inaweza kuwa muundo na msingi wa kuchukua hatua kadri tunavyosonga mbele na tunatumai Myanmar na jumuiya ya kimataifa wanaweza kushirikiana kwenye suala hili."

Naye rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Oktoba, Balozi Francois Delattre wa Ufaransa amewaeleza waandishi wa habari kuwa..

image
Balozi Francois Delattre wa Ufaransa.(Picha:UM/Video Capture)
(Sauti ya Balozi Delattre)

“Sasa ni lazima kuendelea kuongeza shinikizo kwa mamlaka za Myanmar ili matangazo yao ya awali sasa yawe vitendo thabiti kwa kuanzia na kuacha ghasia, kuweka fursa kamili ya usaidizi wa kibinadamu na wakimbizi warejee nyumbani.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mathew Raycroft amesema wanachotaka ni..

image
Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mathew Raycroft (Picha:UM/Video Capture)
(Sauti ya Balozi Rycroft)

“Jana tumemsikia Aung San Suu Kyi akitangaza mawazo yake ya jinsi ya kujenga mustakhbali mpya wa jimbo la Rakhine. Tutakuwa tunafuatilia kwa karibu anapobadili maneno yake kuwa matendo.”

Kamisheni hiyo ya ushauri ilichapisha ripoti yake ya kwanza tarehe 23 mwezi Agosti mwaka huu.

Mwezi Septemba mwaka huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliwasilisha barua kwa Rais wa Baraza la Usalama ili wajumbe wachukue hatua kukomesha kile kinachoendelea nchini Myanmar ambacho alikifananisha na uteketezaji wa kabila.