Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya raia bado wamekwama Raqqa Syria

Maelfu ya raia bado wamekwama Raqqa Syria

Mapigano yanayoendelea katika jimbo la Raqqa nchini Syria yamewakwamisha maelfu ya watu ambao wameelezea hali ya taharuki wakati mkakati wa majeshi ya serikali ukiendelea kutaka kuwafurusha wanamgambo wenye itikadi kali wa ISIL.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limezitaka pande kinzani kuruhusu raia waliokwama kwenye mapambano hayo kuondoka, likisema wako katika hatari ya kifo endapo hawatapata fursa ya kutoka kwa usalama katika eneo.

Limeongeza kuwa waliofanikiwa kutoroka wanaelezea kuzorota kwa hali mjini humo, huku huduma za maji, chakula, madawa na umeme zikizidi kuwa adimu.

Shirika hilo limesema mapigano yanayoendelea pia katika jimbo la jirani la Deir-ez-Zour yamesababisha zahma kubwa, watu zaidi ya 100,000 wakilazimika kukimbia makwao katika wiki ya kwanza ya mwezi huu.

Wakati huo huo UNHCR inasema imefanikiwa kufikisha msaada wa kibinadamu kwa familia zaidi ya 3,000 kwenye kijiji cha Hama Magharibi mwa nchi hiyo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.