Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maajabu ya roboti Sophia, azungumza na binadamu

Roboti aliyepatiwa jina la Sophia ni miongoni mwa  ubunifu wa hali ya juu kwenye akili bandia.
UN /Manuel Elias
Roboti aliyepatiwa jina la Sophia ni miongoni mwa ubunifu wa hali ya juu kwenye akili bandia.

Maajabu ya roboti Sophia, azungumza na binadamu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yana fursa kubwa ya kuchagiza mchakato wa utekelezaji wa maalengo ya maendeleo endelevu au SDGs endapo changamoto zake zitashughulikiwa ipasavyo.

Kauli hiyo imetolewa na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed kwenye mjadala uliofanyika leo makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuhusu fursa na changamoto za maendeleo ya teknolojia. Akizungumza katika mjada huo ambao pia umehudhuriwa na Sophia roboti aliye mithili ya binadamu amesema, “endapo maendeleo ya teknolojia hayatodhibitiwa vyema yana hatari ya kuongeza kiwango kilichopo cha kutokuwepo kwa usawa,.”

Hivyo nini basi kifanyike kuhakikisha akili hii bandi ya kiteknolojia inatumika vyema kwa faida ya wote? Bi Amina amesema, "inahitaji sisi binafsi na kwa pamoja kujifunza ni vipi tukumbatie uwezo wa teknolojia na kutafakari kwa ubunifu jinsi ya kutumia nyenzo hii kushughulikia changamoto kubwa za wakati huu.”

image
Roboti Sophia kwenye ukumbi wa ECOSOC Umoja wa Mataifa kulikofanyika mjadala kuhusu maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kuchagiza utekelezaji wa SDG's. Picha na UN News Kiswahili/Patrick Newman.

 

Amesema wanazuoni, serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi zinapaswa kushikamana kukuza uwezo wa teknolojia lakini pia kuwa makini na athari nyingi tunazopaswa kuepuka kwani teknolojia mpya zinaweza kufaidisha maisha ya mamilioni ya watu duniani.

Kisha Bi Amina akamgeukia roboti Sophia na kumuuliza nini kifanywe na Umoja wa Mataifa kusaidia mamilioni ya watu wasio na nishati ya umeme na intaneti duniani? Sophia hakutafuna maneno akimnukuu mwandishi mashuhuri wa masuala ya sayansi na teknolojia akajibu “William Gibson kuna wakati alisema siku zijazo zimeshawasili, ila hazijagawanywa sawia, lakini habari njema kuhusu akili bandia au (AI) inatoa matokeo zaidi kwa kutumia rasilimali chache. Hivyo tukiwa makini na kujikita katika matokeo ya ushindi kwa wote, akili bandia itasaidia kugawanya sawia rasilimali za dunia zilizopo kama chakula na nishani wakati binadamu wakiendelea kukumbatia uwezo wa teknolojia hiyo, inawezekana kwamba kila kitu ikiwemo teknolojia kitakuwa kimegawanywa sawia.”

Bi Amina amesisitiza kuwa ushawishi wa teknolojia katika jamii uamriwe na matendo ya binadamu na sio mashine.