Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za kisasa za utabiri wa hali ya hewa kubainishwa Iceland

Mbinu za kisasa za utabiri wa hali ya hewa kubainishwa Iceland

Shirika la hali ya hewa duniani, WMO litatumia mkutano wa jumuiko la ncha ya kaskazini, Artic Cirle kuonyesha mipango yake ya kuimarisha jinsi ya kutabiri hali ya hewa kama njia mojawapo ya kukabili mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo ya ncha ya kaskazini na ile ya kusini duniani.

Mkutano huo utaanza Ijumaa huko Iceland ambapo Mkurugenzi Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi yatokanayo na utoaji wa hewa chafuzi hayasalii kwenye maeneo ya ncha ya dunia bali husambaa ulimwenguni kote.

Amesema joto katika ncha ya kaskazini mwa dunia limeongezeka maradufu na kusababisha barafu kuyeyuka, kupungua kwa barafu ya baharini na hata maeneo  yaliyofunikwa na theluji.

Kwa mantiki hiyo watatumia jumuiko hilo linaloleta pamoja wawakilishi wa serikali, wanataaluma na mashirika ya kiraia kuonyesha mbinu za kisasa za utabiri wa hali ya hewa na ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa jamii na mazingira.