Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ridhieni mkataba unaopinga hukumu ya kifo -OHCHR

Mataifa ridhieni mkataba unaopinga hukumu ya kifo -OHCHR

Leo Oktoba 10 ni siku ya kupinga hukumu ya kifo , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi kote duniani kukomesha ukatili. Selina Jerobon na taarifa kamili.

(TAARIFA YA SELINA)

Bwana guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesisitiza kwamba hukumu ya kifo haina nafasi katika karne 21, kwani ni ukatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Nayo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, imetaka mataifa yaridhie mkataba unaopinga hukumu ya kifo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Rupert Colville amesema mwezi uliopitaMadagascar ilikuwa taifa la 85 kuridhia mkataba huo na Gambia ilitia saini.

Aidha ametaja hatua ya mataifa mengine matatu ikiwemo Togo, Jamhuri ya Dominica na Sao Tome na Principe ambao wamekuwa wanachama tangu 2016 kama muhimu katika kutokomeza hukumu ya kifo kote ulimwenguni.

(Sauti ya Rupert)

“Tuna matumiani kwamba hatua hizi zitachagiza mataifa mengine kutokomeza hukumu ya kifo, tungependa kushawishi mataifa yote kuridhia mkataba na kuonyesha dhamira yao katika utokomezwaji wa hukumu ya kifo.”

Ameongeza kwamba wataendelea kusaidia juhudi zote katika mwelekeo huo na kukumbusha kwamba OHCHR inapinga matumizi ya hukumu ya kifo katika mazingira yoyote.