Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maeneo ya vijijini yana mchango mkubwa katika maendeleo:FAO

Maeneo ya vijijini yana mchango mkubwa katika maendeleo:FAO

Mamilioni ya vijana wanaotarajiwa kuingia katika soko la ajira kwenye nchi zinazoendelea katika miongo ijayo, wameaswa kutokimbia umasikini vijijini badala yake wasaidie kuinua sekta ya kilimo. Flora Nducha na tarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Wito huo upo katika ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo FAO iliyochapishwa leo ikisema maeneo ya vijijini yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo kupitia uzalishaji wa chakula na sekta nyingine.

Ripoti hiyo “Hali ya chakula na kilimo 2017” inasema kukiwa na asilimia kubwa ya watu masikini wanaoishi vijijini katika nchi zinazoendelea, ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDG’s mnamo mwaka 2030 itahitajika kufufua umuhimu wa vijijini uliopuuzwa kwa muda mrefu.

Maeneo ambayo idadi kubwa ya watu wataingia kwenye soko la ajira yametajwa kuwa ni nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na kusini mwa Asia. Andrea Cattaneo ni afisa wa masuala ya uchumi wa FAO mjini Roma.

(ANDREA CUT)

Mabadiliko yanafanyika Kusini mwa Asia na Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara, idadi ya watu walioajiriwa katika sekta ya kilimo inapungua kama ilivyo sehemu zingine duniani kupitia maendeleo, hata hivyo watu ambao wanaondoka katika kilimo na kuondoka vijijini wanaingia katika kazi za sekta isiyo rasmi na yenye ujuzi mdogo, hii ni tofauti kubwa ikilinganishwa na hapo nyuma ambapo kupitia ukuaji wa viwanda , watu wengi walikuwa wanaingia katika sekta ya viwanda."

Ripoti inakadiria kwamba ifikapo mwaka 2020 idadi ya watu duniani wenye umri wa kati ya miaka 15-24 inaongezeka kwa watu milioni 100 na kufikia watu bilioni 1.3.