Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warohingya zaidi wazama baharini wakikimbia ghasia Myanmar

Warohingya zaidi wazama baharini wakikimbia ghasia Myanmar

Zahma inazidi kukumba waislamu wa kabila la Rohingya wanaokimbia ghasia nchini mwao Myanmar ambapo katika tukio la karibuni zaidi watu 13 wengi wao wakiwa watoto wamekufa maji baada ya boti yao kuzama.

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM limesema boti waliyokuwa wanatumia ilikuwa ya uvuvi na hali ya hewa wakati wa safari yao ilikuwa ni mbaya kutokana na dhoruba kali.

Hadi sasa walinzi wa pwani wa Bangladesh wameopoa miili 13 ikiwemo ya watoto wa kiume saba wenye umri wa kati ya miaka mitatu hadi 10.

Yasemekana boti yao yenye urefu wa meta 20 wakati inaondoka Myanmar nyakati za giza ilikuwa imechukua wakimbizi 60 wakihepa askari wa doria.

Mmoja wa manusura, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane amesema familia yake yote imepoteza maisha kwenye ajali hiyo akiwemo baba yake na mama yake mzazi.