Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikataba mingi ya kutetea haki za wanawake haitekelezwi- Mtaalamu

Mikataba mingi ya kutetea haki za wanawake haitekelezwi- Mtaalamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Dubravka Šimonoviæ,amesema bado mikataba mingi ya kutetea haki za kundi hilo hazitekelezwi.

Bi. Šimonoviæ amesema hayo katika ripoti yake aliyowasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuhusu uwezo wa mifumo ya kimataifa ya kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake.

Ripoti ya mtaalamu hiyo inafuatia utafiti aliofanya kwa zaidi ya miaka miwili kwa mashauriano na wataalamu kwenye nyanja hiyo.

Bi. Šimonoviæ amesema wakati wa mashauriano hayo kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni baina ya Umoja wa Mataifa, wataalamu wa mifumo ya kikanda na mashirika ya kiraia.

Pande moja ilitaka mikataba ya sasa itumike bila kuwa na nyaraka pekee ya kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake, wengine walitaka mkataba wa kimataifa utakaokuwa na nguvu kisheria ilhali wengine walitaka kuwepo na itifaki mpya ya mkataba wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, CEDAW.

Hata hivyo mtaalam huyo amesisitiza kuwa kutotekelezwa kwa mikataba ya sasa kunaweza kushughulikiwa kwa kuunda mpango wa kimataifa wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na utafanikisha lengo dogo namba 2 la lengo kuu namba 5 la malengo endelevu la kuondoa pengo kati ya mikataba ya kimataifa na sera za kitaifa.