Ushindi wa tuzo ya #Nobel ni kiashiria kuwa NGOs zina nafasi- UM

6 Oktoba 2017

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema ushindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa shirika la kiraia, ICAN, linalofanya kampeni dhidi ya silaha za nyuklia ni utambuzi wa juhudi za raia za kutokomeza silaha hizo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Guterres amesema athari hizo za kibinadamu na mazingira zinazoweza kutokea iwapo silaha hizo zitatumika tena, hazikubaliki.

Amesema ni juhudi hizo ambazo mwezi Julai mwaka huu ziliwezesha kupitishwa kwa mkataba wa kwanza kabisa wa kimataifa wenye nguvu kisheria dhidi ya nyuklia.

image
UM yapinga jaribio la nyuklia linaloendelea kutekelezwa na DPRK

Bwana Guterres amesema kutokomeza nyuklia imekuwa ni lengo la Umoja wa Mataifa tangu azimio lake la kwanza mwaka 1946 hivyo kuna udharura wa kufanya kila liwezekanalo ili kumaliza kitisho cha silaha hizo.Naye mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika udhibiti ueneaji wa silaha Izumi Nakamistu, amesema ushindi wa tuzo hiyo kwa taasisi inayohusika na kupinga nyuklia umekuja wakati muafaka.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani hii leo, Bi. Nakamistu amesema ni wakati muafaka kwa kuzingatia tishio la nyuklia hasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK.

(Sauti ya Izumi) 

“Tuzo hii ya amani ya Nobel ina  umuhimu mkubwa sana kwa kuangazia muda wake iliyotolewa na mazingira tunamoishi hivi sasa.”

image
Tuzo ya amani Nobel. Picha: UM

Halikadhalika amesema ushindi wa tuzo ya leo kwa ICAN  ambalo ni shirika la kiraia likiwa na wadau kutoka nchi mbali mbali duniani kuanzia barani Afrika hadi Ulaya una maanisha kwamba…(Sauti ya Izumi)

“Raia mmoja mmoja na mashirika ya kiraia wanasongesha kwa dhati maoni ya umma kwenye medani za kimataifa na kuweka kasi iliyosababisha kupitishwa kwa mkataba wa kutokomeza nyuklia tarehe 7 Julai ambao tulikuwa na hafla ya kutia saini wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha Baraza Kuu.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter