Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon chunguzeni mauaji ya raia na wawajibisheni wahusika:UM

Cameroon chunguzeni mauaji ya raia na wawajibisheni wahusika:UM

Serikali ya Cameroon imetakiwa kuhakikisha vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinajizuia na kuchukua hatua za kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati ikikabiliana na makundi ya waandamanaji.

Wito huo kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa umekuja baada ya Jumapili iliyopita watu 10 kuuawa wakati wa maandamano katika eneo la Kusini Magaharibi na Kaskazini Magharibi ambako kuna wazungumzaji wa Kiingereza.

Ofisi ya haki za binadamu inasema Kwa mujibu wa duru za kuaminika vifo hivyo vimesababishwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi ya vikosi vya ulinzi na hivyo wameitaka serikali ya Cameroon kufanya uchunguzi haraka, unaoaminika, usio na upendeleo na huru ili kuhakikisha uwajibikaji kwa wahusika.

Eneo la Cameroon linalozungumza Kiingereza limeshuhudia mvutano na mlolongo wa maandamano tangu mwaka jana kupinga kile wazungumzaji wa Kiingereza wanachokiona kama ni ubaguzi dhidi yao kwa serikali kuwapendelea wazuingumzaji wa Kifaransa.