Watoto 8000 waliuawa kwenye mizozo mwaka 2016- Ripoti

Watoto 8000 waliuawa kwenye mizozo mwaka 2016- Ripoti

Zaidi ya watoto 8,000 walioko kwenye maeneo yenye migogoro ya kivita, waliuawa mwaka 2016 pekee.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 kuhusu watoto kwenye maeneo yenye migogoro ya kivita, ripoti ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekabidhi leo kwa Baraza la Usalama.

Miongoni mwa nchi zilizotajwa na ripoti hiyo ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Iraq, Somalia, Sudan Kusini, Syria na Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ripoti hiyo pamoja na kutaja idadi hiyo ya vifo, inaeleza kwa kina vitendo vya watoto kuendelea kutumikishwa jeshini, mashambulizi dhidi ya shule na hospitali pamoja na ukatili wa kingono dhidi ya watoto.

Taarifa hiyo iliyotolewa baada ya ripoti kukabidhiwa barazani, inaeleza kuwa lengo la nyaraka hiyo siyo tu kuelimisha jamii kuhusu haki ya msingi ya mtoto bali pia kuihimiza kupiga vita ushirikishwaji wa watoto katika migogoro ya kivita.

image
Nchini Sudan Kusini vita vya wenyewe kwa wenyewe vimefurusha maelfu ya watu na miongoni mwao ni watoto, uhai wao ukiwa mashakani. (Picha:UNIFEED Video)
Katibu Mkuu amehimiza pia pande husika kwenye mizozo kuzingatia wajibu wao wa kulinda watoto na kuheshimu  sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu  na haki ya watoto.

Amesihi pande hizo kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kuboresha ulinzi wa watoto kulingana na azimio la Baraza la Usalama .

Hata hivyo amepongeza serikali na makundi yasiyo ya kiserikali ambayo hivi sasa yamechukua hatua kulinda watoto kwenye mizozo akisihi pande nyingi zaidi ziungane kutekeleza wajibu huo.