Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yaungana na WHO na UNICEF kupambana na utapia mlo

IAEA yaungana na WHO na UNICEF kupambana na utapia mlo

Shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu za atomic IAEA, shirika la afya ulimwenguni WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wanafanya warsha ya pamoja wiki hii ili kubaini pamoja na mambo mengine jukumu la teknolojia ya nyuklia katika kukabiliana na mzigo mara mbili wa utapia mlo, ambapo lishe duni inaenda sanyari na uzito wa kupindukia au utipwatipwa na maradhi yasiyo ya kuambukiza yanayotokana na lishe duni kama vile kisukari na magonjwa ya moyo.

Takwimu za WHO na UNICEF zinaonyesha kwamba watoto wa chini ya miaka mitano ndio walio katika hatari zaidi, milioni 115 ni wamedumaa wafupi kuliko umri wao, milioni 52 wembamba sana kuliko wanavyostahili na milioni 41 wana utipwatipwa.

Warsha hiyo inayoendeshwa na IAEA ni ya kwanza kuandaliwa na mashirika hayo matatu ya kimataifa na imewaleta pamoja takribani washiriki 50 wakijumuisha watafiti, wataalamu wa afya na wafanyakazi wa idara za lishe na maradhi yasiyo ya kuambukiza kutoka nchi 30.

Washiriki hao wanajadili ukubwa wa tatizo, kiini chake, hatua za kushughulikia na njia za kupima kiwango cha utapia mlo na kukabiliana nao.

Pia wanalenga kubaini mapengo ya utafiti na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuchukua hatua za utafiti wa lishe, será na mipango kote duniani.

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha utafiti wa afya na lishe wa IAEA Cornelia Loech ili kukabiliana vilivyo na utapia mlo na utipwatipwa hatua madhubuti zinahitajika sasa na moja ni kutumia njia ya isotopic ya teknolojia ya nyuklia ambayo ni nyenzo inayotumika kuelewa ubora wa lishe na jinsi inavyotumika katika mwili wa binadamu ambapo na matokeo yake yataweza kuwasaidia watunga será kuwa na mipango ya kitaifa.