Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushauri na lishe bora kusaidia kukabiliana na utipwatipwa-WHO

Ushauri na lishe bora kusaidia kukabiliana na utipwatipwa-WHO

Takriban watoto milioni 41 walio chini ya umri wa miaka mitano wana uzito wa kupindukia au utipwatipwa kwa mujibu wa ripoti ya 2016 ya shirika la afya ulimwenguni, WHO.

WHO imesema hayo wakati wa uzinduzi wa muongozo mpya wa kukabiliana na janga hilo la kimataifa ambalo linaathiri watoto kote ulimwenguni huku likiripotiwa kuongezeka kwa kasi katika mataifa ya kipato cha chini na cha wastani huku  nusu ya idadi ya watoto wanaougua utipwatipwa wakiishi bara Asia na robo yao wakiwa bara Afrika.

Muongozo wa WHO unalenga watoa huduma za afya kwa ajili ya kutambua vijana na watoto ambao wanahitaji msaada kwani iwapo hakuna ugunduzi wa mapema kuna hatari ya watoto hao kufa katika umri mdogo kutokana na magonjwa mbali mbali.

Dr Francesco Branca, ni mkurugenzi kitengo cha lishe na afya, WHO.

(Sauti ya Dkt. Branca)

“Kufikia sasa watoa huduma walihitajika kuangalia watoto waliokuwa na changamoto za ukuaji au waliokuwa na lishe isiyokidhi viwango lakini hivi sasa tunawaambia kwamba ni lazima wapime uzito na urefu wa mtoto na kwamba wanaweze kupata watoto ambao wana uzito wa kupindukia na kwamba watoto hao wanahitaji ushauri, kuimarisha unyonyeshaji kwa watoto, na kuwa na  lishe mbadala na lishe bora.”

Dkt. Branca ameongeza kwamba sio tu suala la lishe lakini mazingira waliomo watoto hawa yanapaswa kubadilishwa kwa kuhakikisha matangazo ya vinywaji vinayoongezwa sukari yanadhibitiwa na mlo shuleni unazingatia lishe bora.