Watoto waliotawanywa na volkano Ambae wanahitaji msaada haraka:UNICEF

4 Oktoba 2017

Watu takribani 12,000 wako katika hatari kubwa ya volkano nchini Vanuatu wakiwemo maelfu ya watoto waliohamishwa kutoka  kisiwani Ambae na sasa wanahitaji msaada wa haraka kwenye vituo vya muda vilivyowekwa kwenye visiwa vya jirani.

Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambapo mwakilishi wake kwenye eneo la Pacifiki Sheldon Yett,  amesema kikubwa kinachotia hofu ni kwa maelfu ya watoto waliolazimika kukimbia makwao kuwa katika makazi salama.

Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa serilikali ya Vanuatu UNICEF inajitahidi kuhakikisha watoto hao wanapata huduma za msingi ikiwemo maji safi na huduma za usafi mashuleni.

UNICEF inasema zaidi ya wanafunzi 3000 wakiwemo 2000 wa shule za msingi na 1000 wa sekondari hivi sasa hawako shuleni na wanahitaji kusajiliwa katika shule za jirani kwenye maeneo ya Maewo, Pentecost na kisiwa cha Santo

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud