Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu ya mzozo dhidi ya warohingya itapatikana Myanmar- OCHA

Suluhu ya mzozo dhidi ya warohingya itapatikana Myanmar- OCHA

Mratibu Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa, OCHA, Mark Lowcock amesema chanzo cha mzozo dhidi ya wakimbizi wa Rohingya kiko Myanmar na lazima suluhu yake ipatikane nchini humo humo.

Bwana Lowcock amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh baada ya kujionea hali halisi inayokumba wakimbizi hao.

Amesema kinachotakiwa hivi sasa ni kuhakikisha kuwa hali ya sasa haikomai na kuwa janga kubwa linaloambatana na mlipuko wa magonjwa.

(Sauti ya Lowcock)

image
Mkuu wa OCHA Mark Lowcock akiangalia maeneo ambako makazi ya muda ya wakimbizi yametapakaa kwenye kambi ya wakimbizi ya Kaputalong nchini Bangladesh. (Picha:Unifeed Video)
“Kiini cha janga hili kama mnavyofahamu kipo Myanar na hivyo suluhu lazima ipatikane Myanmar. Watu nusu milioni wamekimbilia Bangladesh katika kipindi cha wiki sita au zaidi na tumetaka kufika hapa kuelewa kile kilichotokea na kuona hali halisi kwenye kambi na kinachoendelea katika operesheni za usaidizi.”

Mkuu huyo wa OCHA amesema kadri wimbi la wakimbizi linavyoongezeka, kambi nazo zimezidiwa uwezo akisema ,..

(Sauti ya Lowcock)

“Mazingira kwenye kambi yanatisha. Tunahitaji kuchukua hatua zaidi kusaidia kuliko sasa. Leo nimetangaza usaidizi wa dola milioni 12 kutoka mfuko wa dharura wa CERF ili kuimarisha operesheni. Lakini bado tunasihi marafiki zetu kwenye jamii ya kimataifa waongeze usaidizi.”

Kwa mujibu wa OCHA, idadi ya eneo ambalo linatumia huko Bangladesh kuhifadhi warohingya ambao wengi wao ni waislamu ni sawa na viwanja 889  vya mpira wa miguu.