Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa dola milioni 36 kuimarisha jamii nchini Yemen

Mradi wa dola milioni 36 kuimarisha jamii nchini Yemen

Benki ya Dunia na shirika la chakula na kilimo duniani wamezindua mradi wenye thamani ya dola milioni 36 ili kusaidia harakati za kuondokana na njaa nchini Yemen.

Fedha hizo ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, zitawezesha wakazi 630,000 wa maeneo ya vijijini nchini Yemen wakiwemo wanawake kuongeza uzalishaji wa kilimo na hivyo kuweza kuhimili madhila yatokanayo na mzozo unaoendelea nchini humo.

Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa FAO na pia mwakilishi wa shirika hilo kwa ukanda wa Afrika Kaskazini na Mashariki ya karibu Abdessalam Ould Ahmed amesema mradi huo wa miaka mitatu utakuwa na manufaa makubwa ya kibinadamu kwa Yemen.

Amesema kwa kuwa kilimo ni moja ya sekta muhimu za kiuchumi Yemen, kuimarisha seka hiyo kutaongeza uwezo wa watu kupata chakula lakini pia kushiriki kwenye shughuli za kujipatia kipato.

Nchini Yemen hivi sasa watu wapatao milioni 17 wanakabiliwa na baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa chakula, na kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani.