Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake tunaweza hivyo tuchukue hatua- Inspekta msaidizi Annah

Wanawake tunaweza hivyo tuchukue hatua- Inspekta msaidizi Annah

Mshindi wa tuzo ya kimataifa ya polisi mlinda amani mwanamke, Annah Chota kutoka Zimbabwe amesema mtandao wa wanawake walioanzisha huko Abyei umeleta nuru katikati ya mazingira hatarishi.

Chota ambaye ni mkuu wa kitengo cha usawa wa kijinsiana masuala ya watoto kwenye kikosi muda cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa huko Abyei, UNISFA, eneo linalogombewa na Sudan na Sudan Kusini amesema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Amesema kwa kuwa eneo hilo la Abyei halina taasisi za serikali za kusimamia masuala ya haki na usawa wa kijnsia kwa hiyo…

(Sauti ya Annah)

“Mtandao wa wanawake tulioanzisha ni wazo ambalo nimelitoa nchini mwangu Zimbabwe ambapo si mtandao wa wanawake polisi bali tulilazimika kusaka jukwaa ambalo kwalo tutatumia kupitisha ujumbe tunaotaka kwa wanawake na jamii kuhusu usawa wa jinsia na pia ukatili wa kijinsia na kingono.”

image
Polisi mlinda amani mwanamke kwenye moja ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa. (Picha:UN /Marco Dormino)
Chota ambaye ni Inspekta msaidizi wa polisi akaenda mbali zaidi kilichomhamasisha kujikita katika masuala ya usawa wa kijinsia..

(Sauti ya Annah)

“Kutokana na ubaguzi wa mtoto wa kike niliokumbana nao utotoni niliazimia kutia shime katika chochote ninachofanya ili kuchangia kuondoa fikra potofu za vizingiti kwa mtoto wa kike za kuweza kushindana na mtoto wa kiume iwe shuleni au sehemu ya kazi.”

Anna ambaye ni polisi wa kwanza mwanamke kutoka Zimbabwe kushinda tuzo hiyo akawa na ujumbe kwa wanawake..

(Sauti ya Annah)

“Watu wengi waliofanikiwa, wamekumbwa na vikwazo mara nyingi lakini bado wanasimama na kujitazama na kupata ari mpya na kusema watafanya tena. Kwa hiyo kwangu mimi naamini kuwa kama wanawake tayari tunatekeleza majukumu mengi, na hii ni dalili kuwa hata kwenye ulinzi wa amani tunaweza na tunaweza kufanya mengi.”

Tuzo hii inatambua mafanikio ya maafisa polisi wanawake wanaohudumu kwenye Umoja wa Mataifa na imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2011.