Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen iko katika hatihati ya zahma ya kibinadamu-IOM

Yemen iko katika hatihati ya zahma ya kibinadamu-IOM

Wakati baa la njaa na mlipuko wa kipindupindu vinatishia kuighubika Yemen , mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM William Lacy swing anayezuru nchi hiyo leo ameutaka uongozi wa taifa hilo kutoa fursa mara moja ya kuwafikia watu na misaada ya kibinadamu ili kuokoa maisha.

Amesema ingawa hali inaonekana kuwa shwari katika mji mkuu Sana'a na mpishempishe katika mitaa ya mji huo ikiendelea ukweli ni kwamba inafunika hali halisi ya madhila yanayowakabili watu wa Yemen.

Tayari asilimia 80 sawa na watu milioni 21 wanahitaji msaada kutokana na miaka kadhaa ya vita huku wakishuhudia mashambulizi ya anga na mabomu kila uchao.

IOM inasema watu hao milioni 21 wakiwemo pia wahamiaji hawajui mlo wao unaofuata utatoka wapi , mfumo wa usafi umesambaratika  na mamilioni ya watu hawana huduma ya maji safi.

Bwana Swing anasema serikali ina wajibu wa kuhakikisha fursa ya kibinadamu inapatikana ikiwepo kufungua uwanja wa ndege ili kupitisha misaada na dunia ina wajibu wa kuwasaidia watu wa Yemen.

Vita vinavyoendelea vimekuwa kikwazo cha kufikisha misaada ya kibinadamu na kuchangia kwa kiasi kikubwa utapiamlo na mlipuko wa magonjwa.