Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tauni yatikisa Madagascar, WHO yachukua hatua

Tauni yatikisa Madagascar, WHO yachukua hatua

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linaongeza kasi ya kukabili ugonjwa wa tauni uliotikisa Madagascar ambao umesababisha vifo vya watu 21 na wengine 114 wameambukizwa tangu kisa cha kwanza kiripotiwe mwezi Agosti mwaka huu.

Ugonjwa huo wa tauni umeripotiwa katika mji mkuu Antananarivo na miji mingine ya bandari ambapo serikali imethibitisha aliyefariki dunia hivi karibuni ni raia wa Ushelisheli aliyekuwa ziarani nchini humo.

Hivi sasa mamlaka za afya zinasaka watu ambao walikuwa na makaribiano na mtu huyo ili wapatiwe dawa ili kuzuia maambukizi.

Mwakilishi wa WHO nchini Madagascar Dkt. Charlotte Ndiaye amesema wana wasiwasi ugonjwa huo unaweza kusambaa zaidi kwa sababu tayari umeripotiwa miji mingine na kipindi cha sasa ni cha mlipuko wa magonjwa.

Amesema wanafanya kila jitihada kusaidia serikali ikiwemo uratibu na wahudumu wa afya.

Tayari WHO imetoa dola 300 000 kusaidia operesheni hizo na inaomba zaidi dola milioni 1.5 ili kufanikisha harakati hizo.

Tauni unaotokana na vimelea vinavyoishi kwenye mwili wa panya na huenezwa na nzi anayebeba vimelea hivyo kutoka kwa panya na pia mgonjwa wa tauni anaweza pia kusababisha maambukizi.