Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSTAH yazindua sanamu ya amani

MINUSTAH yazindua sanamu ya amani

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Haiti, MINUSTAH umezindua sanamu ya amani iliyoundwa kwa kutumia masalia ya silaha zilizopokonywa kutoka kwa magenge yaliyokuwa yamejihami. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Uzinduzi huo umefanyika ikiwa imesalia wiki mbili hadi MINUSTAH ihitimishe kazi zake nchini humo ambapo silaha hizo zilipokonywa kutoka kwa magenge hayo na hatimaye kuharibiwa na polisi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi mjini Port au Prince, Haiti, Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo na mkuu wa MINUSTAH Sandra Honore amesema..

(Sauti ya Sandra)

“Umoja wa Mataifa unazindua sanamu hii ya amani na kuzindua kikaragosi  “Ochna kwa  Nirva. Kwa sherehe hii tunaazimia kukidhi wajibu wetu wa kuendeleza maadhimisho ya siku ya amani duniani yaliyofanyika tarehe 21 mwezi Septemba”

Naye Bwana Thermidor ameeleza alichofanya hadi kupata sanamu hiyo.

image
Sanamu ya amani iliyozinduliwa na MINUSTAH ikiwa kwenye moja ya bustani kwenye mji mkuu wa Haiti, Port au Prince. Sanamu hii imetengenezwa kwa kutumia masalia ya vyuma vilivyotokana na silaha. (Picha:Unifeed Video)
 “Nilitumia mabaki ya silaha, niliyaunganisha yote halafu nikayochoma na nondo ambayo iliwezesha kuwa na sanamu kubwa kama hii. Unaona ni malaika anayefanana na binadamu mwenye kichwa cha ndege na mabawa nyuma akiashiria umoja na amani.”

MINUSTA ilianza majukumu  yake Haiti mwezi Juni mwaka 2004 kufuatia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosambaa nchini humo.

Majukumu yake yalikuwa ni pamoja na kurejesha amani, kuweka mazingira ya utulivu na kusongesha mchakato wa kisiasa.