Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumieni vipaji vya wazee kufanikisha ajenda 2030- UM

Tumieni vipaji vya wazee kufanikisha ajenda 2030- UM

Leo ni siku ya wazee duniani ambapo ujumbe wa mwaka huu unataka jamii iangazie kusonga mbele huku ikitumia vyema vipaji, mchango na ujumuishaji wa wazee.

Hatua hiyo inaendeleza azma ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha kuwa kila mkazi wa dunia anafanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ya kuona kwamba hakuna anayeachwa nyuma.

Umoja wa Mataifa unasema mara nyingi uzee unaenda sambamba na mhusika kubaguliwa au kutengwa na jamii yake ilhali mchango wa wazee ni muhimu katika kusongesha jamii.

image
Nchini Burkina Faso, mzee huyu anadhihirisha kuwa eliimu haina mwisho na bila shaka itamsaidia si yeye pekee bali pia jamii yake. (Picha:UNDP/BurkinaFaso)
Nalo shirika la afya duniani linatumia siku ya leo kupazia sauti umuhimu wa kuhakikisha huduma za afya zinakuwa jumuishi ili kulinda maslahi ya wazee.

WHO imesema ujumbe huo unazingatia kwamba ifikapo mwaka 2050 mtu 1 katika kila watu 5 atakuwa ni mzee.

Ingawa idadi ya wazee inaongezeka, WHO inasema bado mfumo wa sasa w afya duniani hauko tayari kuhudumia wazee.

Mathalani katika nchi zilizoendelea ni asilimia 41 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 65 walikumbwa na madhila katika kusaka huduma za malezi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus anasema ili mustakhabli uwe bora mfumo wa afya ni lazime uwe jumuishi ukihakikisha kuwa kuna huduma za malezi kwa wazee na wanazipata popote pale walipo.

Amenukuu mwongozo mpya wa shirika hilo kuhusu huduma jumuishi za malezi kwa wazee akisema unapendekeza huduma zinazopatikana kwenye jamii akisema zitasaidia kubadili anguko la huduma hizo sambamba na kudorora kwa afya ya mwili na akili kwa wazee.