Ukalimani na utafsiri wachagiza diplomasia UM

30 Septemba 2017

Leo ni siku ya kimataifa ya utafsiri na ukalimani wa lugha ambapo Umoja wa Mataifa unaisherehekea kwa mara ya kwanza.

Hatua ya leo inafuatia azimio namba  71/288 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 24 mwezi Mei mwaka huu wa 2017 baada ya kutambua nafasi ya ukalimani na utafsiri katika kusongesha misingi ya chombo hicho chenye wanachama 193.

Siku ya leo inawalenga wataalamu wa lugha ambao wana dhima muhiu ya kuleta pamoja mataifa na kuwezesha mashauriano, mazungumzo na maelewano baina ya mataifa na hivyo kuendeleza amani na usalama duniani.

Akizungumzia siku hii, mkuu kitengo cha utafsiri wa lugha ya Kiingereza moja ya lugha sita rasmi kwenye Umoja wa Mataifa Katherine Durnin, ameelezea vile ambavyo wanazingatia ueledi na umakini wanapofanya kazi yao ya utafsiri na ukalimani.

image
Katherine Durnin, mkuu wa kitengo cha utafsiri wa lugha ya kiingereza kwenye Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/Elizabeth Scaffidi)

Amesema wanahakikisha wakati wa mijadala ya hoja yoyote ile, wajumbe wote wanaelewa  ujumbe mmoja sawia, na hivyo kuendelea na mjadala katika lugha yao.Bi. Durnin amesema ni kwa njia hiyo, wajumbe wote wanaweza kuafikiana kwa kuzingatia tafsiri au ukalimani unawaweka wote katika ngazi moja ya kuelewa hoja.

Alipoulizwa kuhusu matumizi ya programu za kompyuta za kutafsiri. Bi. Durnin amekiri kuwa zinasaidia lakini hata hivyo bado haziwezi kuchukua nafasi ya mtafsiri au mkalimani kutokana na ukomo wake kuoanisha mantiki ya lugha.

Nyaraka za Umoja wa Mataifa huchapishwa katika lugha rasmi sita za chombo hicho ambazo ni kiarabu, kichina, kiingereza, kifaranysa, kirusi na kihispanyola.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter