Guterres aingiwa wasiwasi na kinachoendelea Cameroon

29 Septemba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu kile hali inayoendelea nchini Cameroon ikiwemo matukio ya hivi karibuni ya ukosefu wa usalama.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametaja matukio hayo kuwa ni pamoja na mzozo huko Bamenda na Douala pamoja na kuongezeka kwa hofu na mvutano kwenye maeneo ya Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi mwa nchi hiyo yanayotumia lugha ya kiingreza.

Yaelezwa kuwa jamii kwenye maeneo hayo wamepanga kutumia tarehe Mosi mwezi ujao ambayo ni siku ya uhuru wa Cameroon, kuhamasisha maandamano ya kutaka kujitenga na maeneo mengine ya nchi hiyo ambayo yanazungumza lugha ya kifaransa.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu anasihi mamlaka za Cameroon kuendelea na jitihada za kushughulikia machungu ya jamii zinazozungumza lugha ya kiingereza nchini humo. Halikadhalika amesihi mamlaka ziendeleze hatua za kusongesha maridhiano ya kitaifa yenye lengo la kusaka suluhu ya kudumu ya mzozo huo ikiwemo kusuluhisha chanzo chake.”

Katika Mkuu amesema anaunga mkono kuendeleza umoja na mamlaka ya kitaifa nchini Cameroon akisihi pande zote kujizuia na vitendo vinavyoweza kusababisha ongezeko zaidi la ghasia.

Amesema anaamini kuwa mazungumzo ya dhati na shirikishi kati ya serikali na jamii zilizoko maeneo hayo ya Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi ndio njia bora zaidi ya kuendeleza umoja wa kitaifa na utulivu nchini Cameroon.

Bwana Guterres amesema yuko tayari kusaidia jitihada hizo ikiwemo kupoitia ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Afrika ya Kati, UNOCA.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter