Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaanzisha vituo vipya vya kujifunza kwa watoto wakimbizi wa Rohingya

UNICEF yaanzisha vituo vipya vya kujifunza kwa watoto wakimbizi wa Rohingya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limetangaza linaanzisha vituo vipya vya kujifunza 13,000 kwa ajili ya watoto wakimbizi wa Rohingya walioingia Bangladesh kutokea Myanmar.

Hivi sasa UNICEF inaendesha vituo 182 vya kujifunza katika kambi zinazohifadhi Warohingya kwenye makazi ya Cox’s Bazar na vimesajili watoto 15,000. Inatarajia kuongeza idadi ya vituo hivyo kutoka 1500 na kufikia 200,000 mwakani.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa UNICEF Bangladesh Edouard Brigbeder ni muhimu sana kwa watoto hao ambao wameathirika vibaya na machafuko yanayoendelea kupata fursa ya elimu katika mazingira mazuri na salama.

Amesema sio muhimu tu kwa kuwapa watoto hao mazingira ya kawaida wanayoyahitaji bali pia waweze kujenga mustakhbali wao.

Vituo hivyo vinatoa elimu ya awali kwa watoto wa umri wa miaka 4 hadi 6 na elimu ya msingi isiyo rasmi kwa watoto wa umri wa miaka 6 hadi 14 na wanafundishwa masomo ya Kibengali, Kiingereza, hisabati, Kibama, sayansi, Sanaa, na nyimbo.