Kinachoendelea Myanmar kinaweza kuibua misimamo mikali- Guterres

28 Septemba 2017

Janga la kibinadamu linaloendelea huko Myanmar likiambatana na idadi kubwa ya waislamu wa kabila la Rohingya kukimbia nchi hiyo siyo tu linatoa fursa ya kuimarika kwa misimamo mikali ya kidini bali pia inaweka hatarini makundi mbalimbali ikiwemo watoto.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres wakati akilipatia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo tathmini ya kile kinachoendelea Myanmar tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi tangu tarehe 25 mwezi uliopita.

(Sauti ya Guterres)

“Tumepokea simulizi za kusisimua mwili kutoka kwa wale waliokimbia, hususan wanawake, watoto na wazee. Shuhuda hizi ni kiashiria cha ghasia kali na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo ufyatuaji wa silaha bila kuchagua na uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini na ukatili wa kingono.”

image
Wazee, watoto na wanawake wametoa simulizi za kusisimua na kuweka bayana mateso wanayokumbana nayo huko jimboni Rakhine nchini Myanmar. (Picha:Unifeed Video capture)

Katibu Mkuu amesema ingawa serikali ya Myanmar imedai kuwa operesheni za kijeshi zilikoma tarehe 5 mwezi huu baada ya wimbi kubwa la watu kukimbia jimbo la Rakhine ambako wakazi wengi ni kabila la Rohingya….(Sauti ya Guterres)

“Bado wimbi la watu kukimbia limeendelea, na kuna ripoti ya kwamba vijiji vya waumini wa dini ya kiiislamu vimechomwa pamoja na uporaji wa mali zao na vitisho.”

Katibu Mkuu amewaeleza wajumbe kuwa Umoja wa Mataifa utasalia mdau wa karibu wa Myanmar katika kusaka suluhu ya suala hilo la dharura na kwamba..

(Sauti ya Guterres)

“Hatuna ajenda nyingine zaidi ya kusaidia Myanmar isonge katika ustawi wa wananchi wote. Hatuna maslahi zaidi ya kuona jamii zote zinafurahia amani, usalama, ustawi na kuheshimiana. Natoa wito kwa Baraza la Usalama lishikamane na kusaidia jitihada za kumaliza haraka janga hili.”

Tarehe pili mwezi huu Katibu mkuu Guterres aliandikia barua Baraza la Usalama akisihi liimarishe juhudi kusaka suluhu ya Myanmar ambapo tayari chombo hicho kimekutana mara nne ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja kujadili Myanmar.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter