Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boko Haram wasababisha zaidi ya nusu ya shule huko Borno Nigeria kufungwa

Boko Haram wasababisha zaidi ya nusu ya shule huko Borno Nigeria kufungwa

Mashambulizi ya Boko Haram huko Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria yamesababisha zaidi ya asilimia 57 ya shule kwenye jimbo la Borno kufungwa licha ya kwanza muhula mpya wa shule umeshaanza. Patrick Newman na ripoti kamili.

(Taarifa ya Patrick)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema hali hiyo inatokana na kwamba tangu kuanza kwa janga hilo mwaka 2009, walimu zaidi ya 2,200 wameuawa na 19,000 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Justin Forsyth ambaye amekamilisha ziara yake ya siku tano huko Maiduguri mji mkuu wa jimbo la Borno amesema kwa sasa watoto wapatao milioni Tatu kwenye eneo hilo wana mahitaji ya dharura ya elimu, wakati huu ambapo wanaishi kwa hofu kubwa.

(Justin Forsyth),

 “Hapa jimbo la Borno, mapigano yamesambaratisha karibu nusu ya shule, maelfu ya walimu wameuawa, kwa hiyo ni lazima tusaidie watoto waweze kujifunza na hilo ni muhimu kama ilivyo kazi ya kuokoa maisha tunayofanya katika afya na kukabili utapiamlo.”

Hata hivyo amesema baadhi ya watoto wanaoishi kwenye kambi, angalau kwa mara ya kwanza wanaweza kujifunza akitolea mfano kambi ya Muna Garage ambako asilimia 90 ya watoto wameandikishwa kwa mara ya kwanza.

UNICEF inatoa wito kwa uchangiaji wa miradi yake ya dharura ya kuokoa maisha huko Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria ikisema miezi tatu ikisalia kwa mwaka kuishi, miradi hiyo ina pengo la asilimia 40 kwa mahitaji ya mwaka huu.