Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warohingya 14 wafariki dunia baada ya boti yao kuzama

Warohingya 14 wafariki dunia baada ya boti yao kuzama

Boti iliyokuwa imebeba warohingya wanaokimbia mateso kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar imezama kwenye rasi ya Bengal na kusababisha vifo vya watu 14.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Bangladesh Edouard Beigbeder amesema idadi kubwa ya waliofariki dunia ni watoto.

Amesema idadi kubwa ya warohingya wanatumia njia zisizo salama kukimbia mateso akisema tukio hili la karibuni zaidi ni ishara kwa jamii ya kimataifa kusaidia harakati zinazoongozwa na serikali ya Bangladesh za kuwasaidia warohingya.

Mwakilishi huyo amesema yaaminika makumi kadhaa ya watu wamepoteza maisha katika safari kama hizo tangu kuanza kwa mzozo kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar mwishoni mwa mwezi Agosti.

Yasadikiwa kuwa katika wiki za hivi karibuni watoto zaidi ya 250,000 kutoka Myanmar wamesaka hifadhi kusini mwa Bangladesh.