Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mimba milioni 25 hutolewa katika hali isiyo salama kila mwaka duniani:WHO

Mimba milioni 25 hutolewa katika hali isiyo salama kila mwaka duniani:WHO

Duniani kote mimba milioni 25 hutolewa katika hali isiyo salama kila mwaka sawa na asilimia 45 ya mimba zote zilizotolewa kati ya 2010 na 2014. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa shirika la afya duniani WHO na taasisi ya Guttmacher uliochapishwa leo na jarida la afya la Uingereza ,The Lancet.

Ikiwa leo ni siku ya utoaji mbimba salama duniani , takwimu hizo zinaonyesha kwamba sehemu kubwa ya utoaji mbimba usio salama au asilimia 97 hufanyika katika nchi zinazoendelea hasa barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Dr Bela Ganatra ,mwandishi mkuu wa utafiti huo na mwanasayansi wa idara ya afya ya uzazi na utafiti ya WHO anasema juhudi zaidi zinahitajika hususan katika nchi zinazoendelea ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa ya dawa za uzazi wa mpango na utoaji mimba salama.

Ameongeza kuwa wasipopata fursa ya dawa hizo na huduma ya utoaji mimba salama kuna athari kubwa kwa afya zao na kwa familia zao na haipaswi kuwa hivyo.

WHO inasema licha ya maendeo ya karibuni ya teknolojia bado mimba nyingi zinatolewa katika hali isiyo salama na kuwafanya wanawake wengi kuendelea kuathirika na kupoteza maisha.