Azimio la kisiasa kuchagiza vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu

27 Septemba 2017

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu, wakati huu ambapo kitendo hicho kinabinya haki za msingi za binadamu hususan wanawake na watoto.

Azimio hilo namba A/72/L.1 lenye kurasa 6 ni sehemu ya utekelezaji wa mpango uliopitishwa na mkutano wa 71 wa Baraza Kuu uliotaka hatua za kutokomeza kitendo hicho.

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema azimio hilo limepitishwa wakati muafaka mamilioni ya wanawake na watoto wanasafirishwa kiharamu ili kutumikishwa jeshini, kwenye ngono au hata utumwani.

(Sauti ya Guterres)

“Sekta lukuki za biashara kwenye nchi tajiri na maskini zinajinufaisha na kitendo hiki kibaya. Kuanzia uzalishaji chakulka hadi bidhaa za walaji, kampuni kubwa zinaguswa na sekta hii.”

Katibu Mkuu amesema jitihada za kutokomeza madhila hayo ziende sambamba na kampeni za kuelimisha jamii ili watu wengi zaidi wafahamu athari zake na waweze kujiepusha na kitendo hicho akisema..

(Sauti ya Guterres)

“Iwapo uhalifu huu utaendelea kuwepo, hatutaweza kuwaeleza vijana kuwa mustakhbali wao utakuwa bora kuliko siku zilizotangulia. Hatutaweza kuwa dunia yenye matumaini na fursa kwa wote na hatutadiriki kujitazama bila kuwa na aibu. Sasa na tusimame pamoja na tuondokane na aibu hii.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter