Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji mimba salama uwe ni haki ya wanawake wote wanaohitaji: UM

Utoaji mimba salama uwe ni haki ya wanawake wote wanaohitaji: UM

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa nchi zote duniani kubadili sheria zinazoharamisha na kuweka vikwazo katika  suala la utoaji mimba na sera za unyanyasaji, kuwaachilia waanwake wote walioko kifungoni kwa makossa ya utoaji mimba na kukomesha unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba.

Wametoa wito huo katika kuelekea siku ya utoaji mimba salama duniani ambayo itakuwa Septemba 28 na huku wakitaka siku hiyo kufanywa kuwa siku rasmi ya Umoja wa Mataifa ya utoaji mimba salama ili kuzisaidia nchi kuhalalisha utoaji mimba na kutoa huduma za afya ya uzazi kihalali, kwa njia salama na gharama nafuu.

Wamesisitiza kwamba uwezo wa wanawake kufanya maamuzi kwa ajili yao na familia zao hasa katika masuala ya uzazi wa mpango isiwe ni marupurupu kwa matajiri tu bali iwe ni haki ya kila mwanamke na msichakna kote duniani, kama ilivyo haki ya afya na uhuru wa kutobaguliwa.

Hivyo katika kuadhimisha siku ya utoaji mimba salama wataalamu hao wamezitaka nchi zote duniani kuhalalisha utoaji mimba na kuhakikisha wanawake wote wanaweza kupata fursa muhimu na ya lazima ya huduma za afya ya uzazi.