Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna udhuru kwa wanaotekeleza unyanyasaji na ukatili wa kingono-UNMISS

Hakuna udhuru kwa wanaotekeleza unyanyasaji na ukatili wa kingono-UNMISS

Hakuna msamaha kwa mfanyakazi yeyote wa Umoja wa Mataifa ambaye atapatikana na hatia ya kutekeleza unyanyasaji na ukatili wa kingono (SEA,) umesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Hayo yamesemwa leo katika uzinduzi wa kampeni ya kuzuia na kukabiliana na uovu wa aina hiyo ikiwa ni moja ya kipaumbele cha UNMISS. Kampeni inaweka kitovuni haki za wahanga na inalenga kuimarsiha upelelezi na kuripoti visa hivyo ikiwemo pia suala la uwazi.

Akizungumza katika wakfu wa mafunzo kwa afisa polisi wa UNMISS kuhusu viwango vya uadilifu na vitendo, mkuu wa kitengo cha vitendo na nidhamu, UNMISS Mumbi Mathangani, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wote kuelewa kwamba vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kingono ni ukiukaji wa haki za binadamu na vinahitaji kushughulikiwa haraka.

UNMISS itasambaza kadi za ‘hakuna udhuru’ ili kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanazingatia viwango vya juu kuepukana na uovu huo. Kadi hizo zitakuwa na taarifa kuhusu kuripoti ukiukaji na kusisitiza umuhimu wa kuripoti vitendo vya ukiukaji ikiwa ni ziada ya mafuzo yanayotolewa kwa walinda amani wote wa Umoja wa Mataifa.