Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yatoa wito wa chanjo kwa ng’mbe kudhibiti ugonjwa wa bumbuasa

FAO yatoa wito wa chanjo kwa ng’mbe kudhibiti ugonjwa wa bumbuasa

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO leo limetoa wito kwa nchi za Ulaya Mashariki na Balkans kutoa chanjo kwa mifugo hasa ng’ombe ili kuwakinga na ugonjwa wa kuambukiza wa bumbuasa ambao huathiri ngozi na kuifanya kuwa na manundu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo, FAO inaonya kwamba hata kwa nchi ambazo hazijaathirika na ugonjwa wa bumbuasa hadi sasa  lakini zinachukuliwa kuwa katika hatari, zinahitaji kutoa chanjo hiyo ili kuepusha hatari ya kuzuka na kusambaa kwa ugonjwa huo ambao unaweza kuwa na athari kubwa kwa wakulima hasa wadogowadogo.

Ugonjwa wa bumbuasa ambao huathiri ng’ombe unatokana na kirusi ambacho huambukizwa kwa kuumwa na mdudu na unaweza kuuwa haraka mifugo, japo hauathiri binadamu.

Ugonjwa huo awali ulikuwa ukiathiri Afrika tu lakini FAO inasema mwaka 2013 ulizuka Uturuki na kisha kusambaa haraka katika nchi tisa za Ulaya Mashariki na Balkans.