Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota Magharibi mwa CAR-OCHA

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota Magharibi mwa CAR-OCHA

Hali ya kibinadamu magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR inaendelea kudorora tangu kuanza kwa mwezi Septemba kufuatia vikundi vilivyojihami kuteka baadhi ya maeneo ikiwemo miji ya Bocaranga na Niem na vurugu hizo zimesababisha idadi kubwa ya watu kufurushwa. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Takriban wakazi 15,000 wengi wa Bocaranga na 8,000 wa Niem wamesaka hifadhi kwenye misitu ambako huduma za kibinadamu haziwafikii.

Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA inasema matukio haya ya kikatili yamechangia watoa huduma kukatisha shughuli zao za misaada.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini CAR, Najat Rochdi ameonya kwamba raia wanaendelea kulipa gharama kubwa kufuatia ghasia zinazotokana na mashambulizi kati ya vikundi vilivyojihami.

Halikadhalika ameonya kwamba uwezo wa jamii wa kutoa misaada ya kibinadamu uko katika shinikizo kufuatia ufadhili hafifu.