Misaada zaidi yahitajika kwa ajili ya Warohingya:UNHCR

26 Septemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetoa wito kwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa kimataifa kuongeza mara mbili juhudi za kuwasaidia wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh.

Wito huo umekuja wakati kukiwa na hofu kwamba hali ya wakimbizi 436,000 walioingia Bangladesh kutoka Myanmar mwezi uliopita inaweza kuwa mbaya. UNHCR imeendelea kupeleka misaada kwa njia ya anga lakini bado haitoshelezi. Adrian Edward ni msemaji wa UNHCE Geneva.

(SAUTI YA ADRIAN)

“Licha ya juhudi zinazofanyika huko , wimbi kubwa la watu wanaosaka usalama linazidi uwezo wa huduma, na hali ya wakimbizi hawa bado haijatengamaa. Wengi wa waliowasili hivi karibuni wameathirika sana kisaikolojia, licha ya kupata hifadhi Bangladesh na bado wanakabiliwa na hali ngumu.”

UNHCR na washirika wengine wa kimataifa wa misaada wanaendelea kuwasaidia wakimbizi hao hususani wasiojiweza kama watoto, wanawake, walemavu na wazee wanaohitaji msaada wa haraka wa malazi, chakula, maji na huduma za afya.

Wakati wa ziara yake juma lililopita nchini Bangladesh kamisha mkuu wa wakimbizi Filipo Grandi amesisitiza umuhimu wa kupata suluhu ya wakimbizi hao kwa kushirikiana na serikali ya Bangladesh.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter