Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la UM #UNGA72 watamatishwa

Mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la UM #UNGA72 watamatishwa

Katika hotuba yake ya kufunga mjadala wa wazi wa kikao cha 72 cha Baraza Kuu la Umoja wa mataifa, Rais wa baraza hilo Miroslav Lajčák ametilia mkazo mambo muhimu ambayo baraza lake limejikita kuyatekeleza wakati wa uongozi wake.

Mambo hayo ambayo ni mapendekezo yaliyotolewa na nchi wanachama wakati wa mjadala wa wazi ni pamoja na kipaumbele katika kuimarisha amani na mbinu za kuzuia machafuko, usawa wa kijinsia na haki za kibinadamu  kwa wote na utekelezaji wa  utawala wa sheria katika nchi ambazo sheria hazizingatiwi.

Bw. Lajcak pia amegusia suala la wakimbizi na wahamiaji akisema dunia ina nafasi ya kipekee kuweka tofauti kando na kuwaona wakimbizi na wahamiaji kama binadamu kuliko ilivyozoeleka.

Pamoja na tofauti  na mitazamo mbalimbali toka kwa wajumbe wa mjadala wa wazi wa kikao cha 72 cha Baraza Kuu Bwana Lajcak amehitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa dunia inabadilika kwa hivyo Umoja wa Mataifa una wajibu wa kulinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusimamia malengo ya maendeleo andelevu au SDGs.

image
Rais wa baraza Kuu Miroslav Lajčák akihutubia Baraza Kuu. Picha: UM/Video capture
Sauti ya Miroslav 

“Wengi wenu katika hotuba zenu mmeweka wazi kuwa suala la tabianchi limekuwa suala kufa na kupona kwa watu, viumbe vyote na nchi zetu. Kumekuwepo na hisia nyingi sana katika kuunga mkono mkataba wa Paris. Pia mmeonyesha msimamo wenu kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa kwa kusema tuna nguvu tukiwa pamoja”.

Mjadala wa wazi ulianza tarehe 19 mwezi huu wa Septemba kwa viongozi na wakuu wa nchi na wawakilishi kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhutubia na kueleza masuala kadhaa ikiwemo changamoto na kile kinachopaswa kufanyika ili kusimamia misingi ya  Umoja wa Mataifa.