Malaysia ilinde utamaduni wake wa stahamala-Mtaalam UM

25 Septemba 2017

Mtaalam maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema Malaysia iko katika hatari ya kupoteza mengi iwapo mamlaka haitachukulia kwa uzito viashiria vya tishio la kupotea kwa desturi ya stahamala nchini humo.

Mtaalam maalumu katika haki za utamaduni, Karima Bennoune amesema Malaysia imeibuka katika kipindi cha miaka mingi cha changamoto ya kujenga jamii jumuishi lakini hatua zilizopigwa zinafaa kutiliwa maanani kwani kuna hatari ya kupoteza sifa hiyo iwapo hatua hazitachukuliwa kukabiliana na changamoto zinazoibuka.

Bi Bennoune, amesema hayo baada ya ziara ya siku kumi ya kutathmini hali halisi iliyobaini msukumo mpya wa kubadilisha uelewa wa dini ya Kiislamu na utambulisho nchini humo ambao unatenga historia jumuishi, unatenga makundi madogo ya dini na unapuuza utofauti wa waislamu wa Malaysia.

Ameongeza kuwa amesikia ripoti za kuweka misingi ya Uislamu katika maeneo mengi ya jamii ambayo huenda ikabadili utamaduni, mavazi hususan kwa wanawake na wasichana walioko shule na hili huenda pia likabadili sanaa, utamaduni, imani za kidini na historia ya nchi.

Mtaalam huyo ametolea pia wito serikali kutathamini na kuhakikisha haki kwa watetezi wa haki ambao mara nyingi hukabiliwa na unyanyasaji.