Guteress alaani mauaji ya walinda amani wa Mali

25 Septemba 2017

Mauaji ya walinda amani watatu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA yaliyotokea jumapili yamelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Shambulio hilo lilitokea wakati walinda amani hao walipokuwa kwenye msafara kuelekea eneo la Gao, ambapo  walinda amani wengine watano walijeruhiwa vibaya.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na serikali ya Bangladesh

na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemnukuu akisema kwamba Umoja wa Mataifa utaendeleza azma yake ya kusaidia juhudi za amani nchini Mali na kukumbusha kwamba Baraza la Usalama limeweka vikwazo dhidi ya wale wanaozuia utekelezaji wa makubaliano ya amani na wanaoshambulia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.