Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio namba 2334 kuhusu Mashariki ya Kati linazidi kusiginwa- Mladenov

Azimio namba 2334 kuhusu Mashariki ya Kati linazidi kusiginwa- Mladenov

Israel imeendelea kukiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2334 ambalo pamoja na mambo mengine linataka nchi hiyo kusitisha ujenzi wa makazi mapya kwenye eneo inayokalia la wapalestina.

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani  huko Mashariki ya Kati Nikolay Mladenov amesema hayo leo wakati akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana jijini New York, Marekani kujadili hali katika ukanda huo pamoja na hoja ya Palestina.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kati ya kipindi cha kuanzia tarehe 20 Juni mwaka huu hadi tarehe 20 mwezi huu, Bwana Mladenov amesema..

(Sauti ya Mladenov)

“Tangu tarehe 20 mwezi Juni, kasi ya ujenzi wa makazi ya Israel kinyume cha sheria ilikuwa ni kubwa kupita kiasi. Huu ulikuwa ni mwelekeo kwa mwaka huu ambapo shughuli za ujenzi zilijikita eneo la Yerusalem Mashariki ambako mipango ilifanyika ya ujenzi wa zaidi ya nyumba 2,3000, ikiwa ni ongezeko kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka mzima wa 2016.”

Bwana Mladenov amesema kuendelea kubomoa makazi ya wapalestina na utoaji wa kauli chochezi kunaendelea kudidimiza matumaini ya amani kwenye eneo hilo la Mashariki ya Kati.

Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya Mladenov)

“Tunasisitiza kwa uthabiti msimamo wa Umoja wa Mataifa kuwa hakuna mbadala wa uwepo wa mataifa mawili kama ilivyopendekezwa mpango wa utatu wa kumaliza kitendo cha kukaliwa kwa Palestina na kusongesha matumaini ya amani.”